Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi ameombwa kuingilia kati suala hilo kwa vile wanahisi kama ofisi ya Meya Kinondoni hili jambo la mgogoro wao wa ardhi wameuingaza kwenye siasa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Boniface Jacob ambae leo hii amezusha balaa kubwa Kata ya wazo kufutia wananchi kushindwa kumuelewa katika hotuba yake.
Mheshimiwa Paul Makonda akiwa amekaa chini pamoja na wakina mama wa Nyakasangwe na Kazaloho siku ya kwanza alipowatembelea kwa ajiri ya kutatua mgogoro huo wa ardhi uliopelekea mauji ya wananchi wasiokuwa na hatia huku wakina mama kadhaa wakijifungua kabla ya siku zao kwa mabomu ya polisi waliokuwa wanatumiwa na watu wenye mashamba kuonea raia.
Na Livingstone Mkoi
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mkutano wa kwanza wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Boniface Jacob katika Kata ya Wazo kwenye mitaa ya Kazaroho na Nyakalekwa nusra usimalizike baada ya wananchi hao kucharuka vibaya.
Mwandishi wa habari hizi ambaye alikuwa mmoja wa watu waliohudhuria mkutano huo alishuhudia tifutifu hilo lililosababishwa na uchelewaji wa kiongozi huyo mkubwa katika Manispaa ya Kinondoni.
Mkutano huo ulianza saa nane mchana wakati wananchi wakifika eneo hilo toka saa moja asubuhi wakiwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo aliyefahamika kwa jina la Peter Bilebela.
Mkutano huo wa kwanza kwa Meya huyo Mheshimiwa Boniface Jacob ulikuwa na ajenda ya kiongozi huyo kuzungumza na wakazi hao kuhusu mgogoro wa ardhi ambao umesababisha vifo vya watu zaidi ya kumi miaka minne iliyopita ulitokana na watu wanaodai kuwa na mashamba kutumia polisi, na mabaunsa kuharibu mali na kuwapiga wananchi.
Hata hivyo mara baada ya Mheshimiwa Boniface Jacob kuwasili eneo la uwanja wa Nyakalekwa CCM akiwa ameambatana na maafisa wa ardhi, akiwemo Diwani wa kata ya Hananasif, Mheshimiwa Kimbita, Diwani wa Kata ya Wazo na wengine moja kwa moja alilakiwa na umati mkubwa wa akina mama waliokuwa na matumaini tele ya kumuona kiongozi huyo kwa mara ya kwanza toka achaguliwe kuwa Meya.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyakasangwe, Peter Bilebela alifuata itifaki zote zinazostahili kwa kumkaribisha Diwani wa Kata ya Wazo ili amkaribishe mgeni rasmi na mara baada ya kumkaribisha Meya, akiwa ameshika kipaza sauti, alianza kuwasalimia wakazi hao na baadae kuwainua Maafisa Ardhi waanze kusema kwa nini zoezi hilo limechukua muda toka uhakiki umalizike.
Hata hivyo, katika hali ya kushtua, mmoja wa Maafisa Ardhi hao ambaye alitakiwa kuzungumzia suala hilo alianza kuongea kwa kubabaika hali iliyowafanya wananchi hao kuanza kunong'ona chini kwa chini na baadae kwa sauti ya juu hadi afisa huyo alipoamua kumpatia kipaza sauti Afisa mwingine wa Ardhi aliyeambatana Mheshimiwa Meya.
Ufafanuzi wa Maafisa Ardhi huo ulionekana kupingwa na wananchi kiasi cha kuchafua hali ya hewa, hali iliyomlazimu Peter Bilebela Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo kufanya kazi ya ziada ya kuwatuliza wananchi wake.
Meya alianza kuzungumzia kuhusu mgogoro huo akisema awali palitokea makosa kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya (DC Makonda) ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kutowashirikisha viongozi wenzake kwenye suala la uhakiki aliofanyika, kauli hiyo pia ilitaarifiwa kama imeingizwa kwenye siasa.
Kwa sababu kipindi Makonda anafanya maamuzi ya kutatua mgogoro huo hakuwa amemshirikisha Mbunge ambaye ni Halima Mdee na viongozi wengine wa Chadema hivyo moja kwa moja wenye uelewa wa mambo walikuwa wameshamuelewa Mheshimiwa Meya huyo alichomaanisha.
Hata hivyo, Meya huyo alizidi kuzungumza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwasihi watu wasiuze tena mashamba wala kuvamia maeneo mengine kwani kufanya hivyo ni kuendeleza migogoro, lakini, Meya huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa wananchi hao wasijione kama wao wana haki ya kumiliki ardhi hiyo kwa vile wenzao upande wa pili wenye mashamba wengine wana hati tayari za mashamba hayo.
Kiongozi huyo wa Kinondoni aliendelea kusema mengi huku mengine yakionekana dhahiri kuwa vijembe kwa Mwenyeketi Peter Bilebela, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, lakini, jambo lililozusha mtafuruku kiasi cha kuwafanya wananchi kushindwa kumvumilia na kuanza kumjibu katikati ya maongezi yake ni pale alipotoa kauli kwamba hadi sasa watu waliofika kwenye ofisi za ardhi wakitaka nao waorodheshwe kwenye majina ya uhakiki imefikia elfu moja.
Kauli hiyo ilionekana kupingwa vikali na wananchi hao pamoja na Mwenyekiti Peter Bilebela na kusababisha Meya huyo kuwa mpole mbele ya umati huo na kuwaeleza watu kama wanauza viwanja zaidi ya mara mbili basi waache kwa vile ana nia njema na wao na anataka hadi mwezi wa Desemba anahitaji wawe wamepata hati zao.
Baada ya hotuba hiyo ya Mheshimiwa Meya, kipaza sauti kilirudi kwa Peter Bilebela Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo na kumsihi Meya pamoja na Maafisa Ardhi kuwa ni lazima wafuate itifaki (protocal) kwani haiwezekani kwa yeye kama Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ambaye ni kama rais wa mitaa hiyo, kujua idadi ya wakazi wake wote na kuwa na orodha ya watu wenye viwanja, hivyo, anashangazwa na hao watu elfu moja walioongezeka toka kwenye ile idadi ya wakazi wake elfu nne anaowatambua.
Hivyo, Peter Bilebela aliwasihi maafisa hao pindi wanapoona watu wanaotaka kuvuruga amani ya mtaa wake baada ya kuona imetengemaa, wawarudishe ofisi za Serikali ya Mtaa ambako wajumbe wote wana orodha ya wananchi wao. Hali hiyo ilitengamaa kwenye mitaa hiyo na amani imerejea mara baada ya juhudi za Mheshimiwa Paul Makonda.
Kufuatia hotuba ya Meya huyo, Maskanibongotz ilishuhudia akina mama wengi wakiangua vilio huku kila mmoja akizungumza lake na wengine wakisema kwa upeo wao wanaona Meya huyo amepokea vibaya taarifa toka kwa watu wake wa chini hasa viongozi wa Chadema ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakimnung'unikia Peter Bilebela wa CCM.
Hata hivyo, wananchi hao wamesema wamemlilia Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Paul Makonda ambaye kiukweli alikuwa upande wao kiasi cha kuwafanya warudishe imani na serikali yao waliyokuwa wanaichukia kwa kushindwa kuwatetea wanyonge. Aidha, wamemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa William Lukuvi kuunda kamati toka Wizarani kwake ili washughulikie suala hilo kwa umakini na kufuata haki.
Wanasema, hiyo inatokana na kuhisi kama mgogoro huo wa ardhi kwa sasa umeingizwa mambo ya siasa ilhali tayari watu wanaojiita wenye mashamba walishaua, walishaharibu mali kwa kuwabomolea watu nyumba zao bila kibali halali cha mahakama, hivyo wanaamini maamuzi pekee yatakayotolewa na Serikali kuu yatakuwa sahihi na wataishi kwa amani kama wenzao wa Chasimba.
Source: Pazia Jeusi
Visit Youtube or Facebook for more info.
Browse » Home
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment