BOWE, LIPUMBA, MBATIA MNANIDAI MIJELEDI...
NA LUQMAN MALOTO
Juzi, nikiwa nimeketi sebuleni natazama taarifa ya habari, upande wa
pili mtoto wangu Nyambo alikuwa anafanya ‘homuweki’ yake. Kila mmoja
alikuwa ‘bize’ na majukumu yake ya kumalizia siku.
Ila yeye
alikuwa ananisumbua, “baba hii ni nini?” Shule afundishwe yeye, majibu
nitoe mimi. Nyambo anadhani baba yake ni ‘jiniaz’, ananiporomoshea
‘viingereza’ vyake “what is this?” Habari kwamba umande ulinitesa
nikatoka nduki hana!
Nilikuwa natazama Televisheni ya Al Jazeera
idhaa ya Kiingereza, labda kwa kuona hivyo ndiyo akadhani ‘kiinglishi’
kinapanda. Nikimwambia sijui mtoto anakuwa mkali, “teacher said you
should help me” hapo ikabidi niwe mkali nikamwambia “tusitukanane mtoto,
ohoo!”
Nikabadilisha ‘chaneli’, nikarudi kikwetukwetu! Si ndiyo
nikakutana na habari moto ya Ukawa kumsafisha Waziri Mkuu aliyejiuzulu,
Edward Ngoyai Lowassa! Mchana wake nilisikia minong’ono kuwa
ameshajiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Hapo
nikaamini safari imekwiva!
Baba mtu nikaanza kupayuka: “Yeees CCM
kwisha, 2015 CCM out!” Mtoto akanihoji: “Unashangilia Lowassa kwenda
upinzani au Ukawa kumsafisha Lowassa?” Nikamjibu: “Hapa ngoma inogile
mwanangu, Matumaini ameondoka, CCM vipandevipande, CCM siwapendi
walimkata Matumaini.”
“Bora wewe huipendi CCM, mimi nawachukia
Ukawa ni waongo sana,” Nyambo alisema kwa sauti yenye ghadhabu, ikabidi
nimrudi: “Wewe fanya homuweki yako achana na haya mambo ya wakubwa,
unapiga kura wewe?”
“Mengine yatapita, hili halipiti baba, Ukawa
waongo sana na ukiendelea kuwatetea, siku nikisema uongo nisikuone
unanishikia fimbo, patachimbika,” alisema akiwa anawaka, akafunga
daftari kwa hasira na kuondoka.
Nikaona dogo anataka kunipanda
kichwani, nikamwita sauti ya kwanza kimya, ya pili hakujibu akawa
anaenda tu, mara ya tatu nikakaza sauti kiume, akaitika, nikamwambia
arudi haraka.
Akaja ‘kinundanunda’, nikamuuliza kinachomtatiza,
maana ‘testi’ yote ya Matumaini kutoka CCM ilikuwa imetoweka kwa ajili
yake. Akanijibu: “Wewe kila siku nikikuongopea unanichapa halafu wengine
wakisema uongo unawashangilia.” Ile sauti ya Nyambo ilikaa kulialia na
macho yalilengwa machozi, kama baba ninayempenda mtoto wangu,
nilijisikia vibaya, ikabidi niwe mpole.
“Kwani hao Ukawa
wamekudanganya nini mwanangu?” Swali langu liliamsha mizuka ya Nyambo,
alikuwa mkali kama pilipili kichaa. “Huyu Profesa Ibrahim Lipumba wa Cuf
si ni yeye aliyesema CCM imewakosea Watanzania kwa kumpa Lowassa fomu
ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea Urais?
“Tena alisema mtu
aliyepaswa kuwa jela kwa kosa la ufisadi anajitokeza kugombea Urais na
anakwenda kuchukua fomu anapewa. Hawa akina James Mbatia wa NCCR-Mageuzi
na Dk. Emmanuel Makaidi, si walikuwa wanatangaza huku na huko Lowassa
fisadi? Leo hii wanamsafisha bila aibu!”
Nilikosa cha kuzungumza
kwa muda nikawa namtazama Nyambo, nikawaza sijui katumwa kunishawishi
nibaki CCM! Alipoona nimekaa kimya akazidi kumiminika: “Siku ile Juni
18, mwaka huu kwenye mdahalo wa wakuu wa vyama vya siasa, ulioandaliwa
na Taasisi ya CEO Roundtable, si ilikuwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan?”
Nikapiga hesabu, nikamjibu ndiyo. Akasema: “Basi Lipumba hakufunga siku
hiyo, maana nilimuona kwenye runinga akiwa amekaza misuli akielezea
jinsi Lowassa anavyostahili kuwa jela, leo hapa anamsafisha, anasema
kama ni mchafu mbona hajapelekwa mahakamani, huyu babu vipi?”
“Homuweki yako umemaliza?” Nilimhoji ili asiendelee kukoroma, mtoto
mdogo anakoroma mbele ya mkubwa, nilimuona ananikata ‘stimu’. Jibu
nililokutana nalo lilinikata maini. Nyambo wa siku hiyo si sawa na wa
siku zote: “Nitafanya homuweki ukiniahidi na hao Ukawa utawachapa kwa
kusema uongo kama vile ambavyo huwa unanichapa nikiongopa.”
Nikamtolea macho, jamani mimi nina ubavu gani wa kuwacharaza viboko
Ukawa! Tatizo la watoto wanadhani sisi wazazi wao tuna nguvu za kupiga
dunia nzima. Alipoona nipo kimya akanisisitiza: “Tena yule Mwenyekiti wa
Chadema Freeman Mbowe na katibu wake Dk. Willibroad Slaa ndiyo uwachape
mijeledi mingi.”
Aliposema hivyo alikimbilia chumbani kwangu,
aliporejea alikuwa ameshikilia nakala tatu za gazeti linalomilikiwa na
Mbowe. “Baba unaona jinsi hawa watu wasivyofaa kuaminika? Hapa Mbowe
anasema Lowassa dhaifu hatakiwi Ukawa kwa sababu ni bubu. Hili lingine
linasema Lowassa anakaribishwa Ukawa.
“Hili la tatu linasema Slaa
amekataa watakaokatwa na CCM kwa sababu ni makapi, Ukawa
hawatasimamisha mgombea aliyekatwa na CCM. Leo naona chereko za Ukawa
kumpokea Lowassa na kumsafisha. Kuna uongo mkubwa kuliko huu?
Kuudanganya umma wa Watanzania.”
Nyambo ndiye alikuwa nyota wa
mazungumzo yetu siku hiyo, aliteleza kama amekanyaga ganda la ndizi:
“Septemba 15, 2007 nilikuwa sijazaliwa ila baada ya kuzaliwa na kukuta
Dk. Slaa anaitwa shujaa, niliamua ‘kugugo’ niuone ushujaa wake ulianzia
wapi.
“Nikakuta aling’ara kwa kuanika majina 11 ya watu
wanaofilisi nchi. Orodha ya Mafisadi, List of Shame! Katika majina hayo
aliyoyataja, Lowassa ni namba tisa na washirika wake Rostam Aziz na
Adrew Chenge pia wamo!
“Katika Uchaguzi Mdogo wa ubunge Arumeru
Mashariki mwaka 2012, Slaa alisisitiza Lowassa ni fisadi na ndiyo maana
baada ya kutajwa kwenye orodha ya mafisadi mwaka 2007 hakwenda
mahakamani. Akasema Lowassa amejijengea ofisi binafsi ya mbunge yenye
thamani ya shilingi milioni 800 wakati wanafunzi wa Monduli wanakaa
chini, vilevile alipora mradi wa maji Arumeru na kuupeleka Monduli.
“Sasa baba huyu aliyetupiwa kashfa zote hizo anasafishwaje leo na watu
haohao? Fisadi papa wa jana, leo amekuwa kamanda, kivipi? Juni mwaka
huu, Slaa aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter jinsi ambavyo Lowassa
hafai kwa sababu ana madoa ya uadilifu.”
Mtoto akachukua
kompyuta mpakato, akatafuta vya kutafuta kisha akanionesha ‘twiti’ za
Slaa, zilisomeka: “Lowassa tumemtaja katika Orodha ya Mafisadi
walioifikisha nchi hii katika hali mbaya kabisa. Kilele kikiwa sakata la
Richmond.”
Nyingine ikasomeka: “Suala kwamba watu wenye madoa ya
uadilifu wanaota Urais wa nchi ni wazi kwamba kupita katika chama chao
si uadilifu.”
Akaniuliza: “Umeona?” Kwa sauti ya iliyokosa
unyoofu nilimjibu: “Ndiyo mwanangu.” Kwa hakika Nyambo alinithibitishia
kuwa yeye ni mzaliwa hasa wa kizazi cha kuhoji. Kwa siku hiyo alinitoa
‘nokauti’ kwa hoja zake nzito. “Sijui shuleni kwao mwalimu huwa
anawapigisha stori za siasa,” niliwaza, maana kwenye madaftari yake
hakuna somo la siasa.
Nyambo katika ubora wake: “Nilisoma pia
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Mashariki, Mabere Marando alimhusisha
moja kwa moja Lowassa na ufisadi wa fedha Benki Kuu kwenye Akaunti ya
Madeni ya Nje (EPA), vilevile Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu
amekuwa mshereheshaji sana wa ufisadi wa Lowassa. Sasa leo tunaona nini?
“Sasa chama kipi ambacho hakizingatii maadili katika kupitisha majina
ya wagombea? CCM au Ukawa? Mtu ambaye kwa zaidi ya miaka nane ameimbwa
nchi nzima kuwa ni fisadi, leo hii anasafishwa kienyeji tu! Eti mbona
hakupelekwa mahakamani, walitaka apelekwe na nani kama waimbaji ni wao
wenyewe?
“Yaani wewe mwenyewe utoe tuhuma halafu baadaye
umsafishe uliyemtuhumu kwa sababu hakupelekwa mahakamani na unaongezea
hakuna mwenye ushahidi aliwahi kujitokeza. Kwa hiyo ulikuwa unatoa
tuhuma za uongo kufurahisha genge? Unajijenga kisiasa kwa uongo! Yaani
baba usipowachapa hawa Ukawa na mimi hunichapi tena.”
Kwa sauti
ya unyenyekevu, nilimwambia: “Basi mwanangu malizia homuweki tukalale.”
Akaja juu: “Nimekwambia simalizii mpaka uniahidi utawachapa mijeledi
Ukawa, waongo sana! Yule Godbless Lema aliwahutubia wananchi Arusha kuwa
kumkataa na kumzomea Lowassa ni jambo lenye heshima kubwa kwa nchi kwa
sababu ni fisadi, leo anatamba kuwa Safari ya Matumaini inaendelea
Chadema, huyu naye ni muongomuongo lazima umchape.
“Wanajitetea
eti Lowassa hakuwa tatizo bali mfumo uliopo CCM, wakati kila siku
walimtaja moja kwa moja kwamba ni tatizo. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,
John Mnyika alisema CCM inamlinda Lowassa kwa sababu upo ushahidi wa
ufisadi wake, leo hii CCM wamemkataa kuwa mgombea Urais, Chadema na
Ukawa wamemkubali, nani anamlinda?”
Nilimwangalia, akanisistiza
nijibu swali. Nikamwambia sijui, akaendelea: “Hujui eeh! Hivi Ukawa
wanaposema tatizo ni mfumo, mfano mtu akiwa anaishi nyumba jirani, kila
siku mnalamika hamlali anawaibia, siku akihamia nyumbani kwenu ndiyo
mnasema tatizo la wizi wake lilisababishwa na nyumba aliyokuwa anaishi?
Baba nijibu utawachapa huwachapi?”
Kwa upole ikabidi nimwambie:
“Nitawacharaza mijeledi waongo sana hao.” Nilijibu hivyo ili kumaliza
ubishi. Akasema: “Hapo sawa, nami namalizia homuweki yangu nikalale.
Usipowachapa hatutaelewana, siyo unaniitikia tu. Na ukiwachapa uwaambie
mimi ndiye nimekutuma.”
By Luqman Maloto.
Imetoka Jambo Leo
Browse » Home
Wednesday, July 29, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment