Thursday, May 21, 2015

OPARESHENI FICHUA MAOVU OFM YAFURAHISHA WANAWAKE ZA WATU, WAUME ZAO WARUDI SAA 12 ZA JIONI NA KUJIFUNGIA NA FAMILIA ZAO WANANCHI WAPONGEZA MAGAZETI YA GLOBAL KWA JUHUDI WANAZOZIFANYA...!



KITENGO maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers ambacho kimeendelea kujiimarisha kiutendaji, katika kuhakikisha kinafanya kazi yake ipasavyo, sasa imetega kamera kupitia mapaparazi wake ambao watakuwa wakizunguka kila kona ya Jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake, Risasi Mchanganyiko linakubapa kinaga ubaga.



Padri wa Moshi alipofumaniwa na kitengo maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) cha Global Publishers.
TUJIUNGE NA KAMANDA
Kamanda Mkuu wa OFM (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama) aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kuona makundi mbalimbali ya kijamii yanazidi kukiuka kimaadili, kuzidisha uhalifu na kwenda kinyume cha sheria wameamua kujidhatiti zaidi, ili kusaidia kuliokoa taifa katika kadhia hiyo.

KAMERA ZAAGIZWA ISRAEL
Alisema kamera hizo zilizoagizwa Israel, zitakuwa zikitawanywa jiji zima la Dar kupitia kwa makamanda wa OFM ambao watarekodi matukio na kutuma makao makuu ya OFM wakati huohuo.

MAKUNDI YATAKAYONASWA
“Ukiangalia mambo mengi sana ya ajabu yanatokea katika jamii yetu, hasa uvunjaji wa maadili, watumishi wa umma wanavunja maadili, waalimu, madaktari, watumishi wa Mungu na makundi mengine ya watu katika jamii yetu wanakiuka taratibu, sasa tumeona tunao wajibu kushiriki katika vita hii kubwa na tunashukuru kwamba kazi zetu zimekuwa zikiungwa mkono na Jeshi la Polisi ambalo tunafanya nalo kazi mara kwa mara,” alisema Kamanda huyo na kuongeza;


Dokta Mambo.
MAENEO YOTE YA JAMII
“Kwa kutambua hivyo, tutakuwa tukirandaranda na kamera zetu katika nyumba za ibada, hospitali, mahakama, masoko, mahoteli, nyumba za kulala wageni, kwenye ofisi za umma na maeneo mengine yote ambayo tunahisi mmomonyoko wa maadili unaweza kutokea. Watu wanadhulumiwa haki zao, watoto wanabakwa, rushwa ya ngono imeshamiri na baadhi ya watumishi wa Mungu wanaharibu sifa nzuri waliyonayo.

WAOMBA SAPOTI YA WANANCHI
Hata hivyo, Kamanda huyo alisema ili jambo hilo liweze kufanikiwa kwa kiwango kinachotakiwa, ni wajibu wa jamii nzima ya watanzania kushirikiana na OFM ambao wanao uwezo wa kufika kila kona ya nchi kunakotendeka uhalifu.

“Kazi ya OFM siyo mafumanizi tu, tunafanya kazi zote zinazosaidia kufichua uovu katika jamii, ukiona gari la serikali limeegeshwa baa wakati au baada ya saa za kazi, tutaarifu, ukiona mtoto mdogo anatumikishwa kazi ngumu, hapelekwi shule, tuarifu. Tutafuatilia na kuutaarifu umma ili hatua stahiki zichukuliwe.

RUSHWA KUKOMESHWA
“Tunajua rushwa inatembea katika mahakama zetu, tunataka kuwaona mawakala wa mahakimu na majaji wanaopokea rushwa kwa niaba yao, tutawapiga picha na kuwaanika, wananchi watupe ushirikiano. Kuna mambo machafu yanafanyika katika hoteli zetu, biashara ya madawa ya kulevya inafanyika huko, tumefika kwenye fukwe zetu, kuna mambo mengi yasiyofaa yanafanyika huko,” alisema Kamanda huyo na kusisitiza ushirikiano wa wananchi ni muhimu kufanikisha azma hiyo.

TUJIKUMBUSHE
OFM ambayo ina zaidi ya miaka mitatu kazini tokea ianzishwe, imeshanasa matukio mengi yaliyosaidia kuibua uozo sehemu mbalimbali nchini, hususan jijini Dar es Salaam, baadhi ya matukio hayo ni lile la daktari mmoja aliyefahamika kwa jina la Dokta Mambo, ambaye alinaswa huko Kawe, akiwa katika jaribio la kutoa mimba.

Awali, OFM ilitonywa kuwa daktari huyo amekuwa na tabia hiyo kwa muda mrefu kiasi cha kugeuka kuwa kero kwa majirani.Katika tukio hilo lililotokea mapema Januari mwaka jana, daktari huyo alikutwa akiwa na vifaa vyake tayari kwa zoezi la kumtoa mimba memba wa OFM aliyewekewa mtego.
MAKAHABA WA CHINA
Hapo kabla, OFM pia ilifumua mtandao wa makahaba kutoka China, waliokuwa wakifanya biashara ya kuuza miili katika mahoteli makubwa na fukwe za Dar, mwaka 2011.

VIONGOZI WA DINI
Aidha, kwa nyakati tofauti OFM ilifichua mafumanizi mengi yaliyowahusisha wachungaji, mapadre, vigogo wa serikali na watu wa kawaida, katika maeneo mbalimbali nchini. Miongoni mwa mafumanizi hayo ni kama lile lililomhusisha mtanzania mwenye asili ya India, aliyefumwa akitaka kufanya mapenzi na msichana aliyekuwa akihitaji ajira.

FATHER NGOWI
Pia lipo fumanizi lililotokea mjini Moshi, likimhusisha Padre wa Kanisa Katoliki,  Father Ngowi ambaye alikutwa akiwa chumbani na mmoja wa waumini wake, ambaye alikuwa mke wa mtu.

TUKIO BICHI
Tukio ambalo halina muda mrefu ni lile linalomhusu padre mwingine wa Kanisa Katoliki, Anatory Salawa, aliyekutwa kichakani wiki iliyopita akiwa na msichana mrembo ndani ya gari, akidaiwa kutaka kufanya naye mapenzi maeneo ya Kurasini jijini Dar. Tukio hilo lilitokea saa saba usiku, katika siku ambayo mvua kubwa ilikuwa ikinyesha.

0 comments:

Post a Comment

.

 

Copyright © MASKANI BONGO Design by Livingstone Mkoi | Blogger Theme by BTDesigner | Powered by seleman king