KUMRADHI KWA PICHA HII: Maskani ya Mungu huyu ndiye mtoto aliyepoteza maisha kwa ezembe wa Manesi wa Hospital ya Palestina
Mama mzazi akihojiwa na Kitengo Maalum Cha Habari za Uchunguzi cha E-fm Radio
Mwandishi wa toka Kitengo Maalum cha habari za Uchunguzi Bw Livingstone Mkoi akisoma kwa umakini vyeti alivyokuwa amepewa mama huyo mara baada ya kuruhusiwa kwenye Hoisptali hiyo ya Palestina
Waziri Mkuu wa Tanzania Mh Pinda ambae amehusishwa na tukio hili kwa kuombwa na watanzania kuamuru kuundwa kamati ya uchunguzi kutokana na tukio hilo la kifo cha mtoto huyo asiyekuwa na hatia
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk.Seif Rashid ameombwa kukatisha vikao vya Bunge Mkoani Dodoma na kurudi Dar kwa ajili ya sakata hili ili wananchi wawezi kurudisha imani kwa Serikali yao.
Mbunge wa Ubongo Mh John Mnyika.
Na Livingstone
Mkoi Mwandishi Habari za Uchunguzi wa
E-FM
Radio
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na kushtua hospitali ya
Sinza-Palestina imekumbwa na kashfa nzito ya kusababisha kifo cha mtoto mchanga
baada ya kutokana na uzembe wa hali ya juu.
Habari zaidi toka kwa mama mzazi wa mtoto huyo
aliyejitambulisha kwa jina la Elizabeth Kimaro, mwenye miaka 40, zinadai kuwa,
tarehe 22 mwezi huu (Machi) alishikwa na uchungu majira ya saa tisa usiku na
asubuhi kulipokucha mdogo wake aliyefahamika kwa jina la Msiyaka alimpeleka hospitali
hiyo ya Palestina kwa ajili ya huduma zaidi.”
Akisimulia kwa majonzi makubwa, mama huyo ambaye ni mkazi
wa Mabibo aliendelea kusema kuwa, akiwa hospitalini hapo, baada ya kupokelewa
na madaktari, alipimwa na kumwambia kuwa, hana tatizo lolote na kwamba
alielekea kujifungua bila shida huku
wakimsisitizia kuwa njia inafunguka vizuri japo alikuwa amekaa muda mrefu bila
kuzaa.
Akaendelea kusimulia kuwa, baada ya kumaliza kumpima,
mama huyo anadai akaendelea na mazoezi mepesi kusubiri mtoto ashuke na
ilipofika muda wa saa tatu usiku, kuna wahudumu waliokuwa wamempokea tangu
asubuhi muda wao ulikuwa umekwisha, wakaondoka na yeye alikabidhiwa kwa dada
mwingine mhudumu wa zamu ya usiku.
Hata hivyo, mama huyo anasema wahudumu wa zamu ya mchana walikuwa
na moyo wa kibinadamu na huruma ya hali ya juu kwani aliwaona wakipigania
kuokoa maisha ya akina mama na watoto wao huku akiwataja majina ya Elizabeth na
Hyasinta.
Mama huyo anasema wahudumu walioachwa zamu ya usiku ni
watoto wadogo wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 na 20 na ndio walionekana
mara moja kuzungukazunguka kwenye wadi ya wajawazito (leba) kuwahudumia waonasubiri
kujifungua huku leba hiyo ikiwa haina umeme kabisa.
Aidha, mama huyo aliendelea kueleza kwa uchungu kuwa,
wakati hayo yanaendelea, wahudumu watu wazima walikuwa wamekaa upande wa pili
wakinywa kahawa na kutafuna kashata licha ya yeye kuwaita mara kwa mara, lakini,
aliishia kujibiwa; “Wewe unapiga kelele tangu umefika hapa, unaitaita tuuu,
kwani mtoto ameshatoka tayari?”
Mama huyo alizidi kusema kuwa, baada ya kuona
amezidi kupiga kelele za kuomba msaada
kutokana na mtoto kuanza kushuka, mkuu wa wahudumu hao alimtuma mhudumu mmoja
binti aende kumtazama na baada ya nesi huyo kufika alimwambia kuwa kama taa hakuna
basi achukuke simu yake ya mkononi atumie tochi imsaidie kumtolea mkojo
uliokuwa umembana sana.
Hata hivyo, nesi huyo kijana alipochukua simu hiyo ili
akachukue mpira na kurudi kwa kutoa mkojo, kabla hajamtoa mkojo, tayari mtoto
alikuwa njiani kutoka na ilibaki kusukuma tu na mtoto alikuwa mzima, lakini,
alikuwa amechoka kutokana na kukaa muda mrefu kwani mtoto ilikuwa azaliwe saa
tatu lakini amezaliwa saa tano na dakika kadhaa.
Mama huyo anaendelea kusema, alikuwa kila akiwaeleza manesi
wamsaidie, walimwambia ajigeuze tu, hata
ubavu, kwa vile mtoto alikuwa anatoka, huku wao wakimalizia kwa vicheko vya
kejeli.
Kadhalika, mara ya pili yule nesi aliporudi alichukua
tochi ya simu yenye mwanga kwani wao hawakuwa na simu zenye mwanga mkubwa (smart
phone) na baada kufika kwa huyo mama, tayari mtoto alikuwa kishazaliwa.
Elizabeth hapa anasema, kwa kweli hili hata akiitwa kwa Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii Dk.Seif Rashid atasema hata kwa kuapishwa
kwa kitabu cha imani yake baada ya yule mhudumu kufika pale na kukuta mtoto
amezaliwa huku akiwa amechoka, alimuokota mtoto na kumuingiza mipira puani kwa
nguvu, basi hapo damu nyingi kama bomba zilianza kumtoka mtoto puani na yule
mhudumu alivyoona hali ile alishtuka na kusema; ‘Mungu wangu’.
Baada ya hapo mhudumu huyo alichukua khanga na kumwambia
eti ngoja ampeleke sehemu ya mwanga huku damu zikiendelea kulowesha khanga na
baada ya kumpeleka mtoto huyo mhudumu huyo alirudi tena na ile simu yake akiendelea
kusaidia akina mama wengine na hakuhangaika naye tena licha ya kuhitaji msaada
wa kukamuliwa damu tumboni ili kutoa uchafu.
“Yaani sikupata msaada wowote, yule binti nesi aliendelea
kuhangaika mwenyewe usiku mzima kwa kuwazalisha akina mama wajawazito wengine,”
analalamika Elizabeth.
Hata hivyo, mama huyo anasema kumbe kipindi mwanae
alikuwa ameshapoteza maisha wala wasimwambie, lakini, cha kushangaza ni baadae aliwaona
wahudumu kama watano wakiwa ‘bize’ na wagonjwa akajiuliza kumbe wahudumu wote
wapo iweje akina mama wapate shida kiasi kile hata kusababisha watoto kupoteza
maisha?
Mama huyo anasema, licha ya uzembe wa wahudumu
kusababisha kifo cha mtoto wake, lakini, pia lawama nyingine anazipeleka moja
kwa moja kwa uongozi wa hospitali kwa kushindwa kuweka umeme hata wa dharura
katika ‘leba’ ikizingatiwa ni mahala muhimu kuwa na umeme wakati wote.
Aidha, mama huyo anadai kuwa, alipomaliza wahudumu hao
walimjibu: “Hili ni tatizo la muda mrefu, hii ndio serikali yenu, kwanza
hospitali hizi hazina vifaa, someni ubaoni walivyoandika wenyewe kwa uzembe wao,
hairuhusiwi kwa mama yeyote mjamzito kutoa rushwa, eti, vitu vyote ni bure! Uchungu
nao ni shilingi ngapi? Eti tusaidiane!!!”
Mama huyo anasema baada ya mwanae kupotea mhudumu huyo
alikuja kumuweka wazi kuhusu kifo cha mtoto na alipomuhoji sababu ya mwanae kufariki, mhudumu aliongopa kuwa
eti mtoto wake alizaliwa akiwa amejisokota shingoni jambo ambalo hakubaliani nalo
kwa kuwa kwake haikuwa mara ya kwanza kuzaa na hata walipokabidhiwa mwili wa
mtoto huyo haukuwa na alama ya kamba kujisokota zaidi ya damu nyingi puani.
Kufuatia tukio hilo, licha ya mama huyo ambaye ni mfuasi
wa ulokole kutaka kusamehe suala hilo, familia yake imemkatalia mama huyo na
kusema watafika nalo mbali ili kukomesha ukatili unaoendelea kwenye hospitali
hiyo. Aidha, kutokana na mama huyo kuwa katika hali ambayo haijatengemaa
kutokana na kifo cha mwanae, alipandwa na presha na hadi sasa bado hali yake ni
mbaya.
Nacho kituo cha E-FM Radio 93.7 kupitia kwa Kitengo Maalum
cha Habari za Uchunguzi, hatua ya awali kimepiga hodi kwa Mganga Mkuu wa hospitali
hiyo, Dokta Luoga ambaye ameshtushwa na
tukio hilo kwa vile alikuwa amepewa ripoti tofauti juu ya kifo cha mtoto huyo na
wasaidizi wake.
“Jamani, haya mbona makubwa, taarifa za kifo cha mtoto
huyo hizi mezani kwangu, lakini, ziko tofauti na haya maelezo ya huyo mama,” alisema
Dokta Luoga ambaye kipindi hicho alikuwa akisikilizishwa sauti ya mama huyo
iliyorekodiwa.
Aidha, mganga huyo baada ya kuandika maelezo hayo,
aliitisha kikao cha dharura na wakuu wa hospitali hiyo wakiwemo wale wa Ustawi
wa Jamii na kusikiliza tuhuma hizo na kuchukua maelezo ambapo maganga huyo
alisema kuwa, apewe muda wa siku mbili tatu afanye uchunguzi kisha atatoa
taarifa ya kiofisi na kama hata yeye atakuwa amehusika kwa uzembe wa namna
yoyote yupo tayari kuchukuliwa hatua na kama ikibainika wasaidizi wake ndiyo
chanzo basi atamuomba Waziri mwenye dhamana kuchukua hatua kali za kinidhamu
dhidi yao.
Kufuatia tukio hilo, baadhi ya wadau wa hospitali hiyo
pamoja na wananchi wameiomba serikali kupitia Waziri wa Afya kuchukua hatua
kali za kisheria wote waliohusika na uzembe wa kifo cha mtoto huyo pamoja na
wale wanaokula rushwa kwa wagonjwa kwani pia, tukio hili limehusishwa na rushwa
ambapo E-FM ina taarifa zaidi juu ya tuhuma hizo za rushwa kwa baadhi ya wahudumu
wa hospitali hiyo.
Pia hata Mheshimwa Waziri Mkuu amehusiswa kwenye ishu hii na kuombwa kuamliwa kuundwa
kamati ya uchunguzi kuhusu uzembe wa kifo cha mtoto huyu na wale wote
watakaobainika wamehusika basi wachukuliwe hatua kali za kinidhamu ikiwa ni
pamoja kufukuzwa ili iwe fundisho wa wahudumu wengine watakaobaki.
Wakati huohuo, Elizabeth, licha ya kupoteza mtoto wake,
amesema anamuomba hata Waziri wa Afya awaongezee mishahara manesi aliowataja
awali (Elizabeth na Hyasinta) kwa utendaji na uwajibikaji wao mzuri wa kazi
kwani hata walipokuwa wanaondoka waliwaaga wagonjwa kwa kuwafariji na kuwatia
moyo hali iliyowafanya baadhi ya wagonjwa kusikitika kwa kuondoka kwao.
Hata msimamo wa familia kuhusu tukio hilo imesema kuwa
kwa sasa bado wanamuhangaikia mama huyo kwani hali yake bado ni mbya kufuatia
kupatwa na mshtuko kuhusiana na kifo cha mtoto wake ambapo licha ya kwamba
alikuwa na matatizo ya pressure na hili ndo limemuongezea hali hiyo na mara
baada ya kupata nafuu basi wako tayari kulifikisha mbali suala hilo ikibidi
hata kwa Mh Rais Jakaya Mrisho Kikwete watafikisha kilio chao.
Hii ndiyo sehemu ya kwanza ya taarifa hii ya kusikitisha
lakini bado tutaendelea kuwataarifu hatua kwa hatu kwani Mganga Mkuu wa
Hospitali hiyo Dokta Luoga ambae ameomba kupewa muda wa kulifanyia uchunguzi wa
kina na kubaini usiku ule ni wahudumu gani walikuwepo pamoja na mkuu wao manesi
kasha atatoa taarifa za hatua zinazostahiri kuchukuliwa dhidi yao.
Pia E-fm Radio 93.7 kupitia kitengo maalum cha habari za
uchunguzi na ndiyo waliovumbua skendo hii ya kusikitisha inaendelea kufanya
jitihada za kumtafuta Waziri wa Afya kwa ili kumfikishia taarifa za Skendo hii
pamoja ushahidi mwingine, lakini shukrani za pekee zimuendee Mwandishi Mkuu wa
Kitengo hicho cha Habari za Uchunguzi ndani ya kituo cha E-fm Radio Bw
Livingstone Mkoi ambae amelifatilia suala hili usiku na mchana kuhakikisha ushahidi
unakamlika hadi habari hii inaruka hewani. Source: E-fm Radio
0 comments:
Post a Comment